Jumatano ya Majivu katika kalenda ya mwaka wa kanisa katoliki ni siku ya kwanza ya kwaresma lakini katika litrujia ya Milano kwaresma inaanza jumapili inayofuata hivyo majivu kupakwa siku hiyo na sio siku ya Jumatano. Jumatano ya majivu ni ishara ya kuanza kwa siku arobaini za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa kwa kujitoa kwake na kufa msalabani kifo cha aibu ili kuichukua aibu yetu. Kipindi hiki hutusaidia kutafakari juu ya mienendo yetu.

Nini maana ya litrujia ya Milano ni litrujia maalum ambayo inatumika katika sehemu kubwa ya jimbo kuu la Milano na katika parokia kadhaa za majimbo ya kandokando nnchini Italia hadi baadhi ya zile za jimbo la Lugano.

Nini maana ya Kwaresma ni kipindi cha mwaka wa kanisa kinacho andaa Pasaka kadri ya kalenda ya litrujia ya madhehebu mengi ya ukristu.

Jina Jumatano ya Majivu linatokana na desturi katika kanisa katoliki ya kumpaka mtu majivu kichwani pamoja na kumtakia maneno ya kumhimiza afanye toba inavyotakiwa na kipindi hicho cha litrujia kinachoandaa Pasaka.

Kwa kawaida siku ya majivu huanza mfungo wa siku 40 kabla ya sikukuu ya Pasaka. Kipindi hicho kinatunza kumbukumbu ya Yesu kufunga chakula siku arubaini jagwani baada ya kubatizwa na Yohane mbatizaji na kabla ya kuanza utume wake mwenyewe.

Jina la Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbani II: na mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Mwaka 600 hivi, Papa Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya Majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresima na akaongeza urefu wa kipindi hiki cha toba hadi siku arobaini.

Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya Majivu kwaajili ya wadhambi waliotubu katika dhambi na waliojulikana na wakati walipoamua kufanya toba ndio waliopakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile Makahaba, Wauaji, Waasi. Ni Kuanzia karne ya 11, Kanisa lilipanua ibada hii na kuwahusisha waamini wake wote na si wadhambi waliotubu tu.

Majivu wakritu hupakwa hutoka katika matawi ya mitende yaliyo tumika jumapili ya matawi ya mwaka jana. Haya majivu hubarikiwa na kuwa kama Visakramenti. Majivu yanapo ashiria toba na majuto pia hutukumbusha wema wa mungu wa kuwa tayari kutusamehe.

Kwa nini tunatumia matawi ya mitende Matawi ya mitende yalimkaribisha yesu yerusalemu akiwa tayari kushikwa kuteswa na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Ni kwa ajili ya dhambi zetu Mungu alimtoa mwanae wa pekee kufa msalabani na hutusaidia kutafakari ili kuacha dhambi.

Kwanini tunapakwa majivu: majivu ni ishara ya majuto. Tunapopakwa majivu katika paji la uso hutusadia kutafakari na kutukumbusha kuwa wanadamu sisi tu mavumbi na mavumbini tutarudi. Hutukumbusha Zaidi kuwa maisha ya hapa duniani tunapita na safari yetu itakamilika pale tutakapoungana na Bwana mwokozi wetu katika ufalme wake. Hayo hufanywa visakramenti kwa kubarikiwa na kanisa. Katika siku za Agano la Kale na pia katika Agano Jipya, Maandiko Matakatifu yanatuelezea mtu alikuwa ametenda dhambi, alivaa nguo za magunia na kujipaka majivu katika mwili wake  Ukisoma kitabu cha isaya 61:3, ester 4:1-3, yeremia 6:26, ezekieli 27:30, mathayo 11:21 na luka 10:13

Kwa nini majivu yapakwe katika paji la uso na si penginepo? Ukisoma Ufunuo 7:3, Ufunuo 9:4, 14:1, Ezekiel 9:4-6 ishara yoyote iwekwayo katika paji la uso huonesha umiliki. Tunapochorwa ishara ya msalaba tuliyochorwa na mafuta matakatifu siku ya ubatizo wetu, hutukumbusha ahadi tuliyoiweka siku hiyo ya ubatizo na kutuita tuishi maisha ya utakatifu

Maneno anayo tamka padre yana maana gani? Wakati padre anakupaka majivu husema” mwanadamu u mavumbi na mavumbini utarudi au tubu na kuiamini injili. Hayo maneno hutukumbusha tunapoelekea kama binadamu. Yanatuelezea kuwa na furaha kwani wakati miili zetu zitarudi mavumbini roho zetu zitaenda mbinguni kuungana na mungu baba. Maandalizi tunayo yafanya wakati wa Pasaka sio maandalizi ya kuelekea mavumbini bali ni ya kuelekea mbinguni, ndio maana tunaambiwa tubuni na kuiamini injili..

Kanisa limekataza nini siku ya Jumatano ya majivu katoka amri ya pili ya kanisa tunakatazwa kula siku ya jumatano ya majivu na kutokula nyama siku ya ijumaa kuu.

Nini mtu analazimika kufunga siku ya jumatano ya majivu na kwaresma? Kila mkritu aliyetimiza miaka 14 na Zaidi anapaswa kufunga kula nyama ijumaa kuu na mwenye Zaidi ya miaka 21 kufunga chakula jumatano ya majivu

Ni katika mfungo ndipo tunaweza kuiga mfano wa Msamaria Mwema, anayejitolea kumsaidia mhitaji bila kuangalia tofauti zao. Tunaposema kujinyima wakati wa kwaresma  ni kujikatalia kitu unachopenda mfano nyama, pombe, muziki, maongezi safari na kadhalika

Wakati wa kwaresma waamini wanapaswa kujitakasa Zaidi kwa kusali kufunga toba na matendo mema

Kuna hatari ya kuingia kipindi hiki cha Kwaresima kwa mazoea. Tukifanya hiyo hatutafaidika lolote kiroho. Wito kwetu sote: kila mmoja akiingia kipindi hiki cha Kwaresma kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yake. Tuitumie kwaresma hii kana kwamba hakuna tena Kwaresma nyingine. Kwa hakika hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kuiona Kwaresma nyingine. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kipindi cha Kwaresma ndio wakati ulikubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tukitumie vema kipindi hiki. Nawatakieni  mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima.

Story by Imelda Lihavi



Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WP Radio
WP Radio
OFFLINE LIVE