Maafisa wa polisi katika kaunti ndogo ya Narok Mashariki, wamemtia nguvuni mwanaume mmoja kwa kumjeruhi vibaya mtoto wa umri wa miaka saba kwa kumchoma kwa panga iliyo moto.
Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Narok mMshariki Jared Okari Marando, alisema mshukiwa huyo Robert Ombaga Odusu, aliripotiwa kumchoma mtoto huyo akitumia panga iliyo moto katika tarehe tofauti wakati mamake mtoto huyo alikuwa hayuko,lakini mtoto huyo aliokolewa na majirani wema siku ya Jumamosi baada ya kumfumania mshukiwa huyo akimdhulumu na kuripoti tukio hilo kwa polisi.
Mtoto huyo anapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Narok, huku mshukiwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Ntulele. Atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumsababishia majeraha mtoto huyo. Hata hivyo mshukiwa huyo alidai kuwa mtoto huyo alikuwa akimwibia pesa na vifaa vingine na hiyo ndiyo sababu ya kumwadhibu.
Sheria ya watoto ya mwaka 2016 iliboresha haki za watoto hapa nchini ikinuia kuwalinda dhidi ya hatari zinazotokana ndani ama nje ya familia. Sheria hiyo inatoa fursa kwa watoto kukua katika mazingira bora ili wawe wananchi wenye maadili mema.
By Lihavi Imelda