Spika wa bunge la seneti Kenneth Lusaka amewaita waziri wa maswala ya mafuta John Munyes na mwenzake wa kawi Charles Keter kufika mbele ya seneti siku ya jumanne juma lijalo, kueleza sababu za kupanda kwa bei ya bidhaa za petroli.
Katikla agizo lake, Lusaka alisema mawaziri hao wawili sharti wafike binafsi, kujibu maswali ya maseneta.
Hayo yamejiri saa chache baada ya tume ya uthibiti wa kawi na mafuta ya petroli humu nchini kuongeza bei ya reja reja ya mafuta na kuibua shutma kali kutoka kwa umma.
Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot aliibua maswala bungeni Jumatano, akitaka waziri wa kawi na tume ya uthibiti wa kawi na mafuta ya petroli humu nchini kufika mbele yao na kueleza sababu za kupanda kwa bidhaa za petroli.
Tume hiyo iliongeza kwa zaidi ya shilingi 7, bei ya reja reja ya mafuta kuanzia jana Jumatano ambapo lita moja ya super, diseli na mafuta taa sasa itagharibu shilingi 134 na senti 72, shilingi 115 na senti 60, na shilingi 110 na senti 82 mtawalia jijini nairobi.
Wakati huo huo, mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Homa bay, Gladys Wanga na seneta wa Kericho Aron cCheruiyot walishtumiana vikali kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na uamuzi wa Jumanne wa kuongezwa kwa bei ya mafuta.
Cheruiyot alijaribu kuliondoa lawamani bunge la seneti na badala yake kulielekezea kidole cha lawama bunge la kitaifa, hasa kamati ya fedha inayoongozwa na gladys wanga.
By Samson Nyongesa