By Imelda Lihavi

Askofu wa Jimbo Katoliki la Kakamega, Rt. Rev. Joseph Obanyi Sagwe, amewashukuru waumini na wageni wote waliohudhuria hafla ya chakula cha pamoja (luncheon) iliyoandaliwa na Kakamega Zone katika Parokia ya Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu, Malava. Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu alisema kuwa kutoa ni moyo, si utajiri, akisisitiza kwamba kila Mkristo amealikwa kuwasaidia wahitaji kulingana na uwezo aliojaliwa na Mungu ili kuendeleza kazi ya uinjilishaji na kuonyesha upendo wa Kristo kwa vitendo.

Katika ujumbe wake, Askofu Obanyi alieleza kuwa Kanisa linapaswa kuwa mfano wa mshikamano na ukarimu, akiwahimiza waumini kuendelea kushirikiana na kusaidiana bila kujali hali zao za kiuchumi. Alisema matendo ya huruma na upendo ndiyo msingi wa kueneza Injili na kujenga jamii yenye mshikamano.

Aidha, Askofu alielezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la vitendo vya wahuni vinavyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini, akisema hali hiyo inatishia usalama wa wananchi, kuvuruga amani na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Aliwataka viongozi wa kisiasa kutanguliza masuala ya amani na usalama badala ya siasa za migawanyiko, akisisitiza kuwa wana wajibu wa kuwaongoza vijana katika njia zinazojenga taifa na kuwazuia kujiingiza katika vurugu na uhalifu.

Naye mwakilishi wa akina mama, Bi. Elsie Muhanda, aliunga mkono ujumbe wa Askofu Obanyi kuhusu tatizo la uhuni nchini. Alisema vitendo hivyo vinaendelea kuhatarisha usalama wa wananchi na kuwataka wazazi, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa pamoja na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kuwalea vijana kwa misingi ya maadili mema ili wajiepushe na vurugu na uhalifu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Wadi ya Chemuche katika Eneo Bunge la Malava, Kaunti ya Kakamega, pamoja na mapadre, watawa, waumini na viongozi mbalimbali wa Kanisa.

sadmin

By sadmin

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WP Radio
WP Radio
OFFLINE LIVE