Gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliffee Oparanya amesikitikia idadi ndogo ya wanafunzi ambao hujiunga na vyuo vya ufundi katika kaunti hiyo licha ya serikali yake kuweka mikakati kupitia kwa wizara ya elimu kwa kutenga shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi kila mwaka ambaye hujiunga na vyuo hivyo huku akiwataka wazazi kutoka kaunti hiyo kukumbatia elimu ya vyuo hivyo kama njia moja ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kujitegemea maishani.
Akihutubu katika uga wa Bukhungu mjini Kakamega kwenye hafla ya kuzikabidhi shule za chekechea vifaa vya kuwasaidia masomoni vikiwemo viti na meza gavana Oparanya amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kiufundi kaunti hii ni ya chini mno tangu mfumo wa ugatuzi uanzishwe ukilinganisha na wale wa shule za chekechea
Kuhusu swala la miundo misingi gavana Oparanya amesema serikali ya kaunti ya Kakamega imejitahidi kuhakikisha ipo ya kutosha ili kupiga jeki masomo shule za chekechea na vyuo vya kiufundi mbali na kuwaajiri walimu zaidi na kuongeza mishahara yao
Ni shilingi milioni 54.5 ambazo zimetumika kutengeneza viti hivyo vitakavyo wafaidi wanafunzi 124,000 kutoka shule mia 266 wa shule za chekechea zilizoko maeneo bunge kumi na mawili ya kaunti hii, shilingi milioni 74 zikitengwa kununua vitabu vya kusoma katika shule za hizo na vyuo vya ufundi, akipongeza vyuo vya ufundi kwa kuutumia ujuzi wao kuunda vifaa hivyo
By Lindah Adhiambo