Hali ya uzuni imetanda katika kijiji cha Kithiruri, eneo la Kianjokoma, kaunti ya Embu baada ya jamaa mmoja kujitoa uhai na kuacha nambari yake ya siri ya mpesa na kueleza jinsi ya kufungua simu yake.
Mwili wa Lawrence Munene wa miaka 24, ambaye alikuwa fundi ulipatikana ndani ya chumba chake cha malazi siku ya Jumatatu.
Dada mdogo wa marehemu alienda kumgongea mlango mida ya saa tatu ili aamke ila hakupata jibu na kisha akamuarifu babake ambaye alivunja mlango wa chumba cha marehemu na kupata mwili wa mwanawe ukiwa umening’inia kando ya kitanda chake.
Munene alikuwa ameandika ujumbe akiaga familia yake na kuomba msamaha kutoka kwa yeyote ambaye aliwahi kukosea. Aliagiza kwamba mbuzi zake zikabidhiwe mtoto wa dadake.
Siku ya Jumatano familia ya marehemu ilisema kuwa waliweza kufungua simu yake ila hawakupata jumbe zozote ambazo ziliashiria sababu zake kujitoa uhai.
Mama wa marehemu, Cecilia Wanja alisema kuwa mtoto wake alikuwa mpole, mnyenyekevu na mkarimu.
Wanja alisema kuwa mwanawe hakuonyesha dalili za shida yoyote na hakusema chochote cha kuashiria kuwa alikuwa na tatizo fulani, jambo ambalo linampa wasiwasi sana.
By Imelda Lihavi