Wananchi walioko maeneo ya mashinani kaunti ya Busia wamehimizwa kukumbatia kwa dhati swala la kilimo ili waweze kuchangia katika ujenzi wa taifa mbali na kujikimu kimaisha.
Huu ni ujumbe wa gavana Sospeter Ojaamong wakati wa kupeana fedha za kufadhili kilimo cha makundi yapatayo 110 ya wakulima kaunti hii ya Busia chini ya mpango wa Kenya Climte Smart Agriculture Project, ambapo amewataka wakulima hao kuekeza vyema fedha hizo kwa manufaa ya wananchi wengine.
Ni kauli iliyoungwa mkono na mgurugenzi wa mpango huo wa Kenya Climate Smart Agriculture Project daktari Allan Ogendo na waziri wa kilimo kaunti hii ya Busia daktari Moses Osiya waliosema kuwa kufadhiliwa kwa miradi ya kilimo kutasaidia kutokomeza swala la umaskini haswa maeneo ya mashinani.
Naye naibu gavana Moses Mulomi amesema kuwa wataanza kupiga msasa ubora wa miradi yote ya kilimo inayofadhiliwa kaunti hii ya Busia ili kuhakikisha inawapa wananchi fursa ya kujinufaisha.
Mkewe gavana Judy Ojaamong amesifia sekta ya kilimo katika kuboresha maisha ya wenyeji wa Busia, akiwataka wenyeji kukumbatia mradi huo kwa faida mara dufu.
Wakati uo huo gavana Ojaamong amepuzilia mbali ripoti ilioorodhesha kaunti ya Busia miongoni mwa kaunti maskini zaidi nchini.
Katika maswala ya siasa gavana Ojaamong ameshikilia msimamo wake wa kumuunga mkono naibu wake Mulomi akitaja baadhi ya wagombezi kuwa wasio stahili.
By Hillary Karungani