Aliyekuwa mwalimu mkuu katika shule ya upili ya Icaciri, Bi Jane Muthoni, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mumewe kinyama, Solomon Mwangi Mbuthi.
Mahakama kuu ya Nakuru ilimpata Muthoni pamoja na mshatakiwa mwenzake Isaac Ng’ang’a almaarufu kama ‘Gikuyu’ na hatia ya kupanga njama ya kumuua mumewe ambaye alikuwa mwalimu mkuu katika shule ya upili ya wavulana ya Kiru baada ya kumshuku kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi wa Mpesa pande za Murang’a.
Wawili hao walikamatwa mwaka wa 2016 baada ya kutuhumiwa kutekeleza mauaji hayo kati ya Novemba 6 na Novemba 11 mwaka huo.Mwili wa marehemu ulipatikana Nov 11, siku 5 baada ya kukosekana, ukiwa umetolewa viungo na kufunikwa na mifuko kwenye kichaka cha Karakuta kilicho Juja, Kiambu.
Inadaiwa kuwa waliomuua walimkamata kabla achukue karatasi za mtihani wa KCSE ambao ulikuwa uanze asubuhi iliyofuata.Ushahidi uliokusanywa na wapelelezi ulidhibitisha kuwa Muthoni alihusika kwenye mauaji hayo pamoja na wengine watatu, Isaack Ng’ang’a, Joseph Kariuki Njuguna na Nelson Njiru Magati.
Muthoni, Ng’ang’a na Njuguna walikamatwa na kushtakiwa ila Njiru hajulikani aliko hadi kufikia leo. Waliposomewa mashtaka, Muthoni na Ng’ang’a walikanusha huku Njuguna akikubali na kupokea kifungo cha miaka saba mwezi machi 2017.
By marseline musweda