Serikali ya kaunti ya Kakamega imetakiwa kuweka mipango kabambe itakayo hakikisha miradi ya kuwasaidia wasiojiweza inawafikia walengwa ili kupigana na lindi la uchochole ambalo limekita mizizi katika kaunti hiyo.
Wakizumgumza baada ya hafla ya kumjengea nyumba ajuza mmoja wa miaka 70 kwa jina Dorina Wanunda ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba ya karatasi katika kijiji cha Ebuchifi eneo bunge la Mumias Magharibi, wanahabari katika kaunti ya Kakamega wakiongozwa na Fredrick Mukhwami wamesema kuwa nyingi ya miradi ya kuwasaidia wasiojiweza katika jamii ikiwemo inua jamii hufeli kutokana na ufisadi huku wakizitaka idara husika kuimarisha mipango yao.
Kauli hii imetiliwa mkazo na mzee wa kijiji cha Ebuchifi wycliffe Kotia ambaye amesema ni mama mmoja tu katika kijiji hicho ambaye amenufaika na mradi wa serikali ya kaunti hii kuwajengea ajuza wasiojiweza manyumba tangu mpango huo uanzishwe.
Mama Dorina kwa upande wake hakuficha furaha yake baada ya kujengewa nyumba huku akisimulia masaibu aliyopitia katika nyumba yake ya awali ikiwemo kibaridi na ukosefu wa usalama
By Richard Milimu