Wito umetolewa kwa serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutathmini upya ushuru unaotozwa bidhaa muhimu ikiwemo bidhaa za mafuta ya petroli ili kuwawezsesha wananchi kurejelea maisha yao ya kawaida hasa wakati huu mgumu wa janga la corona.
Mtafiti wa maswala ya maendeleo kaunti ya Bungoma Justin Wekunda anasema sekta mbalimbali zimeathirika na janga la corona na kupelekea wananchi wengi kupoteza ajira akihoji kuwa kupandisha ushuru kwa bidhaa muhimu kunaathiri mapato ya mwananchi wa kawaida.
Aidha Wekunda amewataka wananchi kujitenga na mashirika ambayo huenda yakatumia wakati huu mgumu kuwafyonza pesa kando na kutaka serikali kuimarisha miundo msingi katika taasisi za elimu.
Amezitaka sekta mbalimbali ikiwemo ya kidini na biashara kuwahusisha vijana kwa maswala ya kijamii ili kujitenga na visa vya maadili potovu.