Biwi la simanzi limetanda katika kijiji cha Shitukhumi  wadi ya Bunyala  Magharibi eneo bunge la Navakholo kaunti ya Kakamega baada  ya mwanaume mwenye umri wa miaka 47 kupigwa teke na mwanawe wa miaka 21 na kufariki papo hapo kwa madai ya kuzozania ugali.

Kulingana na Alfred Uluma  anasema kuwa nduguye ambaye ni mwendazake kwa jina David Juma alikumbana na mauti yake jana usiku wakati alipodai kupewa ugali  uliokuwa  umepikwa kwa unga uliokuwa umenunuliwa  na mwanawe  na kwa hasira akavamiwa na mwanawe kwa kumpiga teke na kuanguka na kufariki papo hapo.

Kwa upande wake Hadija Nekesa  ambaye ni mkewe marehemu amekanusha madai hayo na kusema kuwa mwanawe kwa jina Michael Juma  wa miaka 21 na mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya St.Johns Budonga alitofautiana na babake ambaye alikuwa amelewa baada ya kumuuliza mbona haendi shuleni licha ya kulipa karo kabla ya mshukiwa kumvamia kwa mateke na kumuua.

Kisa hicho kimethibitishwa na naibu chifu wa eneo hilo Issa Machio akisema kuwa mshukiwa ametiwa mbaroni na mwili kuhifadhi katika chumba cha wafu katika hospitali kuu ya kaunti ya Kakamega huku akiwataka vijana kujiepusha na matumizi ya mihadarati na badala yake kuzingatia masomo yao.

Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Navakholo huku uchuguzi  dhidi ya mauaji hayo ukiendelea.

By Linda Adhiambo

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WP Radio
WP Radio
OFFLINE LIVE