Wafanyibiashara wanaouza nafaka na bidhaa zingine katika soko mjini Mumias kaunti ya Kakamega wamesuta hatua ya serikali ya kaunti hiyo kuwataka kulipia liseni ya shilingi elfu nne na mia tano kila mwaka badala ya shilingi thelathini ambazo wamekuwa wakilipia kila siku kama ushuru wa kufanya biashara.
Wakizungumza mjini Mumias wafanyibiashara hao wakiongozwa na Alima Rajab wanadai kuwa hawana uwezo wa kugharimia ushuru huo mpya wa shilingi 4,500 kwani pia wanalipia shilingi elfu moja kwa vibanda ambavyo wanafanyia biashara yao kila mwezi.
Kulingana na wafanyibiashara hao wanasema kuwa tangia ujio wa mkurupuko wa virusi vya corona na kufungwa kwa kiwanda cha sukari cha Mumias biashara yao imedorora na kukata liseni ya shilingi elfu nne na mia tano utakuwa mzigo kwao.
Kwa sasa wanamtaka gavana wa kaunti hiyo Wycliffe Oparanya kuingilia kati kwani watashindwa kulipia wanao karo shule zinapofunguliwa wiki lijalo na hawana mahala mbadala pa kupata pesa.
By Lihavi Imelda