Vijana wa Lugusi kutoka eneo bunge la Malava walitoka sare ya tasa dhidi ya mahasimu wao United Star kwenye mechi ya ligi ya FKF kaunti ya Kakamega.
Mechi hiyo ilisakatwa katika uwanja wa Lugusi huku Eshitari pia wakatoka sare nyingine ya bao moja dhidi ya West Kenya all-stars katika uwanja wa Eshitari eneo bunge la Butere nao Mzalendo wakawalemea One Acre Fund wa Lurambi kwa kuwarindima magoli matatu kwa moja katika uwanja wa mwangaza.
Kwingineko vijana wa golden arrows walikabiliana koo dhidi ya Shitaho kwa kufungana magoli mawili wakati Museno Samba na Ivonda kings pia wakatoshana nguvu ya kufungana bao moja kila mmoja.
Akizungumza na kituo hiki kocha wa Lugusi ambaye pia ni mwakilishi wa vijana katika shirikisho la kandanda nchini FKF kaunti ya Kakamega Enoch Lucheveleli , alishukuru timu zote kwa kuonyesha mchezo wa kuridhisha na pia wasimamizi wa timu hizo.
Wakati huo uo Lucheveleli alikubali sare hiyo ya timu yake ya Lugusi na kuwataka vijana wake kuendelea na mazoezi wakati huu wa likizo ndiposa wafanye vizuri kwenye mechi zingine.